Jumanne, 17 Januari 2017

Ufahamu - Sura ya Kwanza

Sura ya Kwanza


1. Sisi watu tunaishi katika ulimwengu wa damu na nyama. 2. Tunaweza kushirikiana na kujua vitu mbalimbali hapa duniani kwa kutumia milango ya fahamu.  3. Milango ya fahamu ndiyo inayotuwezesha kuingiza taarifa kwenye akili zetu. Kwahiyo kadiri tunavyo ingiza vitu kwenye akili tunapata ujuzi wa kujua vitu mbalimbali vilivyopo duniani.

4. Kadiri ya siku zinavyozidi kwenda taarifa nyingi sana zinakuwa zimesajiliwa kwenye akili zetu. Kitendo hicho kinafanya tuishi katika dunia kwa kutegemea vitu ambavyo tumeingiza kwenye akili kupitia milango ya fahamu.  5. Kitendo hicho kinatufanya sisi wadamu tuishi katika ulimwengu wa dhahania (Virtual World). Kwamba ulimwengu huo unakuwa ni ulimwengu ambao siyo halisi. Unakuwa ni ulimwengu ambao upo kwenye akili zetu kwa kutegemea vitu tulivyoingiza kupitia milango ya fahamu. 6. Kwahiyo tunakuwa hatujui ni mambo gani yanaendelea katika ulimwengu wa roho, maana tunategemea yale tunayoyapata kupitia milango ya fahamu.

7. Wakati tukiwa watoto wachanga tulikuwa karibu sana na ulimwengu wa roho. Lakini tatizo kubwa tulikuwa hatuna uwezo wa kuwasiliana na ulimwengu wa damu na nyama. Maana tunaokutana nao wanakuwa wamejiwekea taratibu zao za kuwasiliana. 8. Kwa kuwa tulikuwa hatujui namna ya kuwasiliana nao basi ilitubidi tuanze kujifunza namna ya kuwasiliana nao. 9. Kitendo hicho kilitufanya tuanze kuzoea mazingira ya ulimwengu wa damu na nyama. 10. Tulianza kufundishwa vitu mbalimbali vya ulimwengu wa damu na nyama. Tulifundishwa taratibu mbalimbali tangu tukiwa watoto wachanga. 11. Jambo hilo lilitufanya tuanze kujitenga na ulimwengu wa roho na kuanza kujengwa katika ulimwengu mwingine.

12. Tulianza kufundishwa sheria na taratibu, tulifundishwa vitu vibaya na vizuri kadiri walivyoona kutufundisha. 13. Tulipoenda kinyume tuliambiwa kwamba sio sahihi tulielezwa kipi ni sahihi na wakati mwingine tuliweza hata kuchapwa viboko. 14. Kuna wakati mwingine tulilazimika kufuata kwa sababu ya kuogopa kwamba tutapewa adhabu. Jambo hilo lilitufanya tufuate bila hata kujua lengo la kile tunachofuata.

15. Tulifundishwa utarabu na imani nyingi kuhusu sisi na ulimwengu wa roho. 16. Mara nyingi tulitishwa na kuogopeshwa, kitendo kilichotufanya tuweze kuwasikiliza wale wanaotufundisha na kuwaamini kwa kiasi kikubwa. 17. Jamii iliyokuwa inatuzunguka yote ilikuwa inaenda kwa utaratibu huo huo. Kwa hiyo hatukuwa na namna yoyote zaidi ya kujitahidi kuonekana tunafuata utaratibu wa jamii. 18. Wakati tunaendelea kukua tulikuwa tukifundishwa mafundisho kulingana na umri wetu. 19. Mfundisho mengine yalihusu tamaduni zetu na mengine yalihusu dunia nzima.

20. Tumejikuta tumejitenga kwa kiasi kikubwa na ulimwengu wa roho. 21. Tumejaza mambo mengi ya ulimwengu wa damu na nyama katika akili zetu. Tumekuwa wategemezi wa ulimwengu huu na tunaishi kwa hofu kubwa. 22. Watu wachache wametumia mwanya huu kujinufaisha na kuendelea kutufumba macho ili tusijue sisi ni akina nani na kwanini tupo hapa. 23. Jambo la muhimu ni sisi kutaka kujua sisi ni akina nani na lengo la kuwepo hapa katika ulimwengu wa damu na nyama ni nini? 24. Unaweza ukajiuliza je, lengo la kuwepo hapa duniani ni kufa tu? 25. Jibu utakosa na hatimaye utaangukia kwenye mafundisho uliyopewa huku ukisahau asili yako ni nini.